Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali haitodharau maoni na ushauri wanaoutoa kuhusu maeneo yenye hofu kwenye mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza leo Juni 20, 2023 katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya chuo cha International Evangelism Centre kilichoko Sakina jijini Arusha, amewataka Watanzania kuendelee kuwa na imani na Serikali pamoja na wawakilishi wao ndani ya Bunge, kwani Serikali imejidhatiti kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi unaoendana na mahitaji ya sasa na kwa kuzingatia manufaa ya kijiografia ya nchi yetu.
Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kwamba bandari haijauzwa, bali Serikali inataka kubadilisha mwekezaji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na tija zaidi.
RC Chalamila: Wanaopanga kuandamana waache mara moja
Amebainisha kuwa pamoja na maboresho yaliyofanyika, hali ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda. “Kwa mfano, wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es salaam ni siku tano ikilinganishwa na wastani siku moja na nusu kwa Bandari za Mombasa na Durban.”
Amesema udhaifu huo uliopo katika bandari hiyo unasababisha meli kusubiri muda mrefu nangani na hivyo kuongeza gharama ambapo kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban shilingi milioni 58 kwa siku.
Waziri Mkuu amesema kitendo cha meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku tano ikilinganishwa na siku moja inayokubalika kimataifa, kinasababisha meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar es Salaam pamoja kuikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo ingesaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi.