Kinywaji cha ‘kuongeza’ nguvu za kiume chapigwa marufuku

0
22

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limepiga marufuku uingizaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa dawa ya asili inayotumika kama kinywaji hususani kwa wanaume na kudaiwa kuongeza nguvu za kiume ambacho kinajulikana kwa jina la Akayabagu.

Baraza limesema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa dawa hiyo, ilifanya uchunguzi wa uingizwaji, usambazaji na usalama wa kinywaji hicho na hivyo kubaini kuwa kinywaji hicho hakijawahi kusajiliwa na baraza, na kugundua kuwa kimechanganywa na dawa ya kisasa aina ya sildenafil (Viagra ama erecto/vega) ambapo ni kinyume na sheria.

Utafiti Mpya: Unywaji pombe wa wastani hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo

“Yeyote atakayekiuka agizo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Pia ikumbukwe kuwa, yeyote atakayepatikana akiwa na kinywaji cha Akayabagu atakuwa ametenda kosa, na ataweza kushitakiwa kwa mujibu wa sheria,” limesema baraza.

Aidha, limepiga marufuku uingizaji, usambazaji, uuzaji na utumiaji wa dawa zinazojulikana kwa jina la ‘vumbi la Congo’ likidai kuwa dawa hizo hazijapimwa ubora na usalama wake, hivyo yeyote atakayepatikana akiwa na dawa hizo atakuwa ametenda kosa na ataweza kushitakiwa kwa mujibu wa sheria.

Mbali na hayo, baraza limeikumbusha jamii kuacha tabia ya kutumia dawa hovyo kwani zinaweza kuleta madhara ya kiafya kwa mtumiaji, pia limewakumbusha waganga wa tiba asili na tiba mbadala kote nchini kuhakikisha wamesajiliwa na baraza pamoja na kutoa huduma bora kwa kufuata sheria.