Rais Samia Suluhu Hassan amesema maboresho yanayoendelea kufanyika katika bandari za nchini yatajumuisha ufungaji wa mitambo ya kisasa itakayosaidia kubaini shehena zinazopitishwa zikiwa na dawa za kulevya.
Ameyasema hayo leo Juni 25, 2023 jijini Arusha wakati akishiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya duniani ambapo amezipongeza asasi za kiraia kwa kazi kubwa inayofanyika katika tiba na uratibu wa kuwaunganisha waraibu wa dawa za kulevya.
“Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa wa masuala ya dawa za kulevya na ihalifu limeeleza kwamba Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kutoka nchi zinazozalisha kwa zaidi ya asilimia 90,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali inaangalia namna ya kufanya ili kuwasaidia kiuchumi vijana waliotoka kwenye uraibu wa dawa za kulevya ili wasirejee tena kwenye matumizi ya madawa hayo, na kuwahimiza wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya watoto wao pamoja na kuchukua hatua kila wanapoona mabadiliko ya kitabia kwa watoto ili kuwakinga kutokana na wimbi hilo.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema katika operesheni maalum iliyofanyika mkoani Arusha kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na wananchi wamekamata na kuteketeza bangi kavu gunia 978 na bangi mbichi gunia 5,465 sawa na tani 615.