Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa wasilisho la maamuzi na maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Dubai katika usimamizi na uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam.
Haya ni mapendekezo 11 yaliyotolewa na kamati hiyo;
1.“Kamati Kuu inalitaka bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta azimio lake la kuridhia mkataba wa uendeshaji wa bandari nchini kwa sababu mkataba huo hauna maslahi yoyote kwa nchi yetu.”
2.“Kamati Kuu inaitaka Serikali kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wote walioshiriki kuingiza nchi yetu kwenye mkataba huu mbovu ambao haurekebishiki na umelidhalilisha taifa letu.”
3.“Kamati Kuu inaunga mkono jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na wananchi mbalimbali nchini kupinga mkataba huo ikiwemo wale waliochukua hatua ya kufungua kesi dhidi ya serikali katika Mahakama Kuu ya Tanzania, mahali popote na sehemu mbalimbali katika taifa letu.”
4.“Kamati Kuu imeazimia kwamba itashirikiana na wananchi katika makundi mbalimbali bila kujali itikadi zao katika kupinga mkataba huu wa uendeshaji wa bandari nchini.”
5.“Mkataba wa bandari pamoja na mikataba mingine ya siri ambayo ni mibovu inayoiingiza taifa kwenye hasara ni chachu ya kuona haja ya kuendelea kutaka nchi yetu kuwa na katiba mpya ambayo itaweka utaratibu wa namna ya bunge na vyombo vingine kupitia mikataba hiyo kwa maslahi mapana ya taifa letu.”
6.“Kamati Kuu imeazimia kwamba ikiwa bunge na Serikali havitachukua hatua kuhusu malalamiko ya wananchi dhidi ya mkataba wa bandari, chama kitaanzisha na kuhamasisha umma kuchukua hatua kali dhidi ya serikali mpaka itakapousitisha mkataba huo.”
7.“Kamati Kuu imeridhika kuwa mkataba huo ni kinyume cha katiba ya nchi, kinyume cha sheria za nchi na kinyume cha sheria za kimataifa.”
8.“Imebaini kwamba hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliofanywa na Serikali na ukawekwa kwa umma kuthibitisha ufanisi au uduni wa bandari na ubora wa DP World ili kushawishi wananchi juu ya ufanisi utakaotokana na DP World.”
9.“Kamati Kuu imejiridhisha kwamba wananchi hawajui asili ya mkataba wa DP World, na wao ndio waathirika wakuu wa maamuzi ya Serikali.”
10. “Kamati Kuu imejiridhisha kuwa hakuna utafiti wowote wa kisayansi unaoonesha njia mbadala za kuboresha ufanisi wa bandari.”
11.Kamati Kuu ya chama chetu kitaunga mkono uwekezaji wowote mkubwa unaotokana na utafiti wa kisayansi, usiohatarisha usalama wa nchi yetu ukiwemo utaifa wetu.