Mwanafunzi wa kidato cha tatu ashikiliwa kwa kudaiwa kumuua mwalimu
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Mohamed Jabir, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Qiblatain Islamic iliyoko Kawe jijini Dar es Salaam baada ya kudaiwa kumuua mwalimu ambaye pia alikuwa Patron wa shule hiyo, Hassan Mohamed.
Akizungumza Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema tukio hilo limetokea Julai 20, mwaka huu alfajiri baada ya mwalimu huyo kuwaamsha wanafunzi ili kuhudhuria ibada ya asubuhi na ndipo mwanafunzi huyo kuonesha kukaidi agizo hilo na kisha kumshambulia kwa kisu.
“Mtuhumiwa huyu alionesha kukaidi, baada ya wenzake kuondoka alipata fursa ya kupata kisu na baadaye kumshambulia mwalimu huyu ambaye alipelekwa haraka kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na baadaye akapoteza maisha wakati akipatiwa matibabu,” amesema Kamanda Muliro.
Aidha, amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linalaani vikali kuporomoka kwa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi ambao wamefikia hatua ya kuwashambulia walimu na walezi wao kutokana na kuhimizwa kutekeleza majukumu yao ya msingi.