Kuandika barua ya kazi ni hatua muhimu katika kutafuta ajira au kuwasiliana na mwajiri. Ni vyema kuzingatia mambo kadhaa ili kuhakikisha barua yako ya kazi inaleta taswira nzuri na kumvutia mwajiri wako ili mwisho akupitishe kwenye hatua ya usaili.
Hapa kuna mambo muhimu ya kuepuka wakati unaandika barua ya kazi;
Kuepuka makosa ya lugha: Hakikisha barua yako inaandikwa kwa lugha sahihi na isiyo na makosa ya sarufi na kisarufi. Unaweza kuomba msaada kutoka kwa mtu mwingine kukagua barua yako kabla hujaituma.
Kutumia lugha isiyo rasmi: Ingawa unataka kuonesha uwezo wako wa kuwasiliana vizuri, ni muhimu kudumisha toni ya kitaalamu na lugha ya heshima. Epuka kutumia lugha ya mazungumzo au maneno yasiyo rasmi. Tumia maneno yanayoeleweka na usimfanye msomaji afikirie ulichomaanisha.
Kutojumuisha mshahara katika barua ya kazi: Hii ni mojawapo ya mambo muhimu ya kuzingatia. Wakati wa kuomba kazi, unapaswa kuepuka kujadili mshahara wako kabla ya mzungumzo rasmi na mwajiri. Kujadili mshahara mapema sana kunaweza kumpa mwajiri picha ya kwamba unaangalia kazi hiyo kama fursa ya kupata pesa zaidi badala ya kuwa na nia ya kufanya kazi na kampuni yao.
Kuandika barua ya kazi isiyo na muundo: Barua ya kazi inapaswa kuwa na mpangilio mzuri. Anza na anwani yako ya mawasiliano, tarehe, anwani ya mwajiri, na salamu ya kumtambulisha mwajiri.
Kutoa taarifa za uongo: Hakikisha taarifa zako ziwe na uwiano na wasifu ulioambatanisha. Ikiwa mwajiri atagundua uwepo wa taarifa za uongo, pengine atakunyima nafasi ya kukuajiri.
Kujigamba sana: Jitahidi kuelezea ujuzi wako na uzoefu kwa njia nzuri, lakini epuka kujigamba sana. Eleza jinsi ujuzi wako utakavyosaidia kutatua matatizo au kuleta mchango katika kampuni.
Kuandika barua ndefu sana: Barua yako ya kazi inapaswa kuwa fupi na yenye kueleweka. Eleza kwa kifupi sababu za kuomba kazi hiyo na uoneshe una uwezo wa kuifanya kwa kiwango gani.
Kutomshukuru mwajiri: Kuhitimisha barua yako na shukrani kwa muda na fursa itakayotolewa kwa kazi hiyo inaashiria heshima na ufahamu wa mchakato wa kutafuta kazi.