Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu kunyongwa hadi kufa Mohamed Njali, kwa kosa la kumbaka na kumuua kwa kumkaba Atika Chesco Kivanule (24) majira ya saa saba usiku wakati mumewe akiwa anatazama pambano la ngumi.
Kesi hiyo imesimamiwa na mawakili wa Serikali, Winfrida Mpiwa na Muzna Mfinanga na kutolewa hukumu na Jaji wa Mahakama hiyo, Angaza Mwipopo.
Mahakama imeeleza kuwa siku ya tukio hilo mshtakiwa alivunja mlango na kuiba simu pamoja na suti, na baadaye kumbaka Atika huku akimnyonga shingoni.
Baada ya kumaliza tukio hilo, akiwa anatoka nyumbani hapo alikutana na shemeji wa marehemu na kuanza kukimbia, baada ya kutoa taarifa polisi mshtakiwa alikamatwa nyumbani kwake akiwa na simu ya marehemu pamoja na suti aliyoiiba.
Mwanza: Watu sita wafariki kwa kugongwa na gari wakifanya mazoezi
Kesi hiyo ilikuwa na mashahidi nane akiwemo daktari aliyeupokea mwili na kuufanyia uchunguzi, ambapo majibu ya kitaalam yalithibitisha kuwa kifo cha mwanamke huyo kilitokana na kukosa hewa kwenye ubongo kutokana na kunyongwa.
Akizungumza mume wa marehemu, Adeline Kileo ameishukuru mahakama kwa adhabu hiyo iliyotolewa dhidi ya kijana huyo.