Mahakama ya Nairobi imemhukumu mchungaji, James Njuguna kifungo cha miaka 70 jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka watoto wadogo wawili wenye umri wa miaka 11 na 14 katika nyakati tofauti kati ya Desemba 24, 2014 na Januari 7, 2015.
Mahakama imebaini kuwa mchungaji huyo alitenda makosa hayo katika eneo la Bondeni, Kajiado Kaskazini mwa Kenya ambapo kosa la kwanza lilimfanya ahukumiwe kifungo cha miaka 50, na kosa la pili lilimfanya ahukumiwe kifungo cha miaka 20 jela na hukumu hizo mbili zitatumika kwa pamoja.
Inadaiwa kuwa Njuguna alikuwa akiwaeleza waathirika wake kuwa majimaji aliyotumia yalikuwa ni damu ya Yesu inayoingia na kuwatakasa. Pia, alidai kuwa sehemu yake ya siri ilikuwa ina mafuta maalum kutoka kwa Mungu.
Uhalifu huu uligunduliwa baada ya mmoja wa waathirika wake kupata ujauzito ambapo katika kipindi cha kusikilizwa kwa kesi hiyo, mchungaji huyo alifanyiwa vipimo viwili vya DNA na kuthibitika kuwa ni baba wa mtoto mnamo mwaka 2015.