Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) limekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kanuni mpya ya usajili inayohusu wachezaji watakaosajiliwa kutoka vilabu vya Tanzania Bara kuingizwa kwenye mfumo kama mchezaji wa kigeni na kukatiwa kibali cha makazi kinachogharimu TZS laki 5.
ZFF imesema hakuna mahali popote katika kanuni ya mashindano ya ZFF 2023/24 sura ya 10 katika kifungu cha usajili na uhamisho wa wachezaji kutoka nje ya Zanzibar ambayo imetaja mchezaji kutoka Tanzania Bara ataingizwa katika mfumo na kukatiwa kibali cha kuishi Zanzibar.
“Mchezaji mwenyeji anayehamia timu ya Ligi Kuu na Daraja la Kwanza Zanzibar atalipiwa shilingi elfu 50. Mchezaji kutoka Tanzania Bara anayehamia katika timu ya Ligi Kuu atalipiwa kiasi cha shilingi 200,000, na anayehamia daraja la kwanza atalipiwa kiasi cha shilingi 100,000.
Na mchezaji anayetoka nje ya Tanzania kuhamia katika Ligi Kuu ya Zanzibar atalipiwa kiasi cha shilingi400,000, na daraja la kwanza atalipiwa kiasi cha shilingi 200,000,” imesema ZFF.
Shirikisho hilo limewaomba wadau wa michezo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kufuata habari zinazotolewa na ZFF au chanzo sahihi ndani ya shirikisho ili kuepuka Habari zisizo sahihi.