Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema kutokana na Tanzania kuwa na fursa mbalimbali za uwekezaji serikali inazingatia vigezo maalum ili kuweza kutambua aina gani ya mwekezaji anayepaswa kupokelewa nchini.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma Waziri Prof. Mkumbo amesema serikali inahakikisha inapokea uwekezaji ambao utakidhi mahitaji ya bidhaa za ndani, aina ya uwekezaji unaoweza kuongeza thamani katika bidhaa au mazao pamoja na kusaidia kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi ili kuongeza fedha za kigeni.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa serikali lazima ijiridhishe kuwa uwekezaji unaotaka kufanyika nchini utasaidia kuzalisha ajira kwa Watanzania, pamoja na kuzingatia uwekezaji ambao utazalisha utajiri kwa Watanzania.
Serikali yaja na mbinu za kuongeza akiba ya dola nchini
Aidha, amesema kwa sasa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo, utalii, fursa ya uwekezaji katika sekta ya viwanda kama vile uzalishaji wa mbolea, dawa za binadamu na mifugo, sekta ya nishati na gesi pamoja na fursa kwenye uchimbaji madini.