ACT Wazalendo yaunga mkono uwekezaji wa DP World, yatoa mapendekezo

0
30

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kinaunga mkono uwekezaji kwenye bandari za Tanzania ili kuziwezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa na tija zaidi kwenye uchumi.

Akizungumzia kuhusu msimamo rasmi wa chama hicho juu ya makubaliano ya IGA kati ya Tanzania na Dubai, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Dorothy Semu amesema bandari za Tanzania zinaendeshwa kwa ufanisi mdogo, hivyo zinahitajika jitihada mahsusi za kuongeza ufanisi na tija ili kuwezesha nchi kufaidika na uchumi wa jiografia yake.

“Tanzania inayo fursa ya kukuza uchumi kwa kutumia bandari, lakini ufinyu wa miundombinu, udhaifu katika uendeshaji na kukosa ufanisi katika shughuli za bandari, vinazuia kutumia hata nusu ya fursa za kiuchumi zinazotokana na bandari. Hivyo basi, suala la uwekezaji (wa umma, binafsi ama ubia) katika bandari zetu halibishaniwi, ama haliwezi kubishaniwa na mtu yeyote yule,” amesema.

Aidha, chama hicho kimetoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuipa pia haki Tanzania juu ya uwekezaji wa DP World kwa kuweka sharti kwa mwekezaji kutofanya mazungumzo au uwekezaji kwa bandari shindani na Dar es Salaam, mfano bandari ya Mombasa, Lamu au Durban, ushiriki wa wananchi au makampuni ya ndani katika uwekezaji, na kutaja muda wa ukomo wa mkataba ili kuondoa taharuki kwa wananchi.

Soma hapa msimamo wa ACT Wazalendo kuhusu makubaliano kati ya Tanzania na Dubai

“Kutokutaja bayana muda wa ukomo wa IGA kunahalalisha maoni kwamba mkataba huu ni wa muda mrefu (kadiri mtu atakavyotaja miaka) au hata wengine kudai kwamba ni wa milele jambo ambalo limeleta taharuki,” kimesema chama hicho.

Hata hivyo, Serikali katika taarifa zake imesema kuwa ukomo wa mikataba utawekwa kwenye mikataba mahsusi ya miradi, na kwamba, kwa sababu utekelezaji wake utachukua vipindi tofauti, isingekuwa sahihi kuweka muda mmoja katika mkataba huo wa ushirikiano (IGA).

Send this to a friend