Mkuu wa Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, Dkt. Julius Ningu ameshitakiwa katika Baraza la Maadili kwa tuhuma za kutoa lugha za matusi, vitisho na kuwaweka mahabusu watumishi wa umma.
Kikao hicho kimeketi chini ya mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Mstaafu Rose Teemba huku upande wa mlalamikaji ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Emma Gelani ambaye amedai kiongozi huyo ailitenda kosa hilo akiwa Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwaweka rumande baadhi ya watumishi akiwemo mtendaji wa Kata ya Rwinga, Mario Fabian.
Kwa mujibu wa Wakili huyo, sheria inamtaka mkuu wa mkoa, au mkuu wa wilaya kutoa maelezo kwa njia ya maandishi kwa Jeshi la Polisi kabla au muda mfupi baada ya kuamuru kuwekwa ndani na kutoa sababu za msingi za kumuweka mahabusi mtuhumiwa.
“Dkt. Ningu hakutoa maelezo yoyote kwa Jeshi la Polisi kuhusiana na kukamatwa watumishi wa halmashauri na mafundi waliokuwa wanatekeleza miradi ya UVIKO-19 katika Wilaya ya Namtumbo, kinyume cha maelekezo ya sheria,” amesema wakili.
Kontawa ajisalimisha jeshini, aomba kujiunga JKT
Kwa upande wa mlalamikiwa amekana kutumia lugha hizo, na kwamba uamuzi wa kuwaweka rumande ulitokana na ushauri wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na si uamuzi wake peke yake.
Baada ya baraza hilo kusikiliza pande zote mbili, mwenyekiti wa baraza amesema watakaa kujadili kwa kina na kisha watatoa taarifa kuhusu uamuzi utakaoamuliwa.