Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema mpango wa bima ya afya kwa watoto wanaojiunga kwa hiari (Toto Afya Kadi) haujafutwa, bali kilichobadilika ni utaratibu wa kuwasajili watoto.
Akikanusha uvumi huo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter), Waziri Ummy ameeleza kuwa utaratibu wa sasa ni kwa watoto kusajiliwa shuleni kwa gharama ya shilingi 50,400 ili waingie wengi wasio wagonjwa na hivyo kuweza kuchangia wachache watakaougua.
“Bima ni sayansi. Huwezi kuwa na bima inayokusanya shilingi bilioni 5; fedha inayolipwa kwa watoa huduma, yaani matumizi, ni bilioni 40. Natamani hizo nguvu za kupotosha zingetumika kuleta ushauri ni vipi NHIF itaweza kuvutia watoto wengi zaidi ambao hawana changamoto za kiafya ili kuweza kulipia wachache watakaopata changamoto za kiafya,” amesema.
Ameongeza kuwa, “kwa sasa Toto Afya Kadi wamesajiliwa watoto laki 2 tu, tuhimizane wazazi/walezi kuwakatia bima ya afya watoto wetu. Naamini wakisajiliwa watoto japo asilimia 10 tu (milioni 3) kwa utaratibu huu basi tunaweza kuhakikisha ustahamilivu na uendelevu wa fao hili.”
Majaliwa amuagiza Naibu Waziri Mkuu kushughulikia upatikanaji wa mafuta
Aidha, Waziri amesema sera ya watoto wa umri chini ya miaka 5 au watu wasio na uwezo kupata msamaha bado haijafutwa, na kwamba hospitali zote za umma zinaendelea kuhudumia watoto wa umri chini ya miaka mitano kupitia utaratibu wa misamaha.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilionesha kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulipata hasara TZS bilioni 204.65 mwaka 2021/22 kutokana na ongezeko la gharama za mafao ya matibabu na gharama za huduma kwa wanachama ambazo hazikulingana na mapato yaliyoongezeka.