TIC: Thamani ya uwekezaji nchini yapanda kwa asilimia 120

0
10

Thamani ya uwekezaji nchini Tanzania imepanda kwa asilimia 120 ndani ya mwezi mmoja, huku sekta ya kilimo ikiendelea kuwa sekta inayovutia zaidi wawekezaji.

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inaonyesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imepanda hadi shilingi trilioni 2.33 mwezi Agosti mwaka huu kutoka shilingi trilioni 1.06 mwezi Julai.

Wakati fedha zilizowekezwa zikipanda, thamani ya uwekezaji uliofanyika kwenye kilimo imeongezeka kwa zaidi ya shilingi bilioni 275.53 mwezi Agosti ikilinganishwa na kiasi kilichowekezwa Julai mwaka huu.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa uwekezaji katika kilimo umeongezeka hadi shilingi bilioni 849.13 mwezi uliopita kutoka shilingi bilioni 571.10 mwezi Julai huku idadi ya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa na TIC mwezi Agosti mwaka huu ikiongezeka hadi 10 kutoka mitatu mwezi Julai.

Kwa mujibu wa TIC idadi ya miradi pia imepanda hadi 58 mwezi Agosti kutoka 40 mwezi Julai. Miradi 58 iliyosajiliwa inatarajiwa kutengeneza nafasi zaidi ya 25,700 za ajira.

Send this to a friend