Rais Kagame atangaza kugombea urais kwa muhula wa nne

0
11

Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema atawania urais kwa muhula wa nne katika uchaguzi wa mwaka 2024 kutokana na wananchi kuwa na imani kubwa na uongozi wake.

Akizungumza na jarida la Kifaransa la Jeune Afrique Jumanne, Rais Kagame amethibitisha kuwa mgombea wa urais wa nchi hiyo na kuahidi kuwatumikia Wanyarwanda siku zote na kadri awezavyo.

Alipoulizwa kuhusu nchi za Magharibi zitachukulia vipi uamuzi wake wa kugombea tena, Rais Kagame amesema, “natoa pole kwa nchi za Magharibi, lakini kile ambacho nchi za Magharibi zinafikiri sio tatizo langu.”

Mwezi Aprili mwaka huu, Rais Kagame alitania kwamba anatazamia kustaafu na kukabidhi madaraka baada ya kukaa kwa takribani miaka 23 madarakani.

Rais Kagame amekuwa Rais wa taifa hilo tangu mwaka wa 2000, huku uchaguzi uliopita 2017 akishinda kwa asilimia 98.8 ya kura mara baada ya kupitishwa kwa kura ya maoni mwaka 2015 iliyoondoa ukomo wa mihula miwili kwa marais.