Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tovuti ya Hifadhi ya nyaraka za aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tano wa Tanzania na mwanadiplomasia mashuhuri, Dkt. Salim Ahmed Salim utakaofanyika Septemba 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Aidha, uzinduzi huo utahudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na viongozi waandamizi kutoka sekta za umma na binafsi, viongozi wastaafu na washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na taasisi za elimu ya juu.
Tovuti hiyo iliyoandaliwa na familia ya Dkt. Salim kwa kushirikiana na Serikali inajumuisha video, picha na nyaraka mbalimbali (kama vile hotuba, nakala za mawasiliano ya kimaandishi na machapisho ya kitafiti) za Dkt. Salim inayoeleza juu ya safari yake ya utumishi wa umma na mchango wake katika mahusiano ya kimataifa na jitihada za ukombozi barani Afrika, pamoja na kuangazia mchango wa nchi za Afrika katika siasa za kimataifa katika kipindi cha mwaka 1960 hadi 2000.