Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Barrick Gold Corporation, Mark Bristow ametoa wito kwa kila mmoja kusaidia kuzuia uvamizi unaotokea mara kwa mara katika mgodi wa dhahabu wa North Mara unaofanywa na makundi ya vijana wenye silaha.
Bristow alitoa ombi hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni uliofanyika siku ya Ijumaa kwenye mgodi huo uliopo eneo la Nyamongo, wilayani Tarime mkoani Mara, ambapo amebainisha kuwa uvamizi huo unaendelea kusababisha athari kubwa kwa taifa ikiwa ni pamoja na majeraha.
Mark Bristow akizawadiwa mbuzi na viongozi wa kimila kutoka koo za Wakurya wilayani Tarime, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii zinazozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
“Nina ombi moja na hili ni kwa kila mmoja wetu, kila mtu. Tushirikiane kukomesha tabia hii mbaya,” amesema Bristow katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali.
Kwa mujibu wa ripoti, mgodi huo umekuwa ukikumbwa na matatizo ya uvamizi na kusababisha usumbufu mkubwa. Ingawa mgodi unalindwa na walinzi binafsi wasio na silaha, mara nyingine polisi hulazimika kuingilia kati wakati hali inapoonekana kuwa mbaya.
Mkuu wa Shirika la Barrick akikabidhi gari kwa viongozi ili kusaidia ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya CSR katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Mgodi wa North Mara unaendeshwa na kampuni ya Barrick Gold kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals Corporation. Pia, kampuni hiyo imewekeza kiasi kikubwa cha fedha nchini Tanzania na inaendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali, na pia inalenga kuajiri watanzania wengi zaidi katika sekta ya madini.