Shirikisho la Ngumi Tanzania (TPBRC) limemfungia kwa muda wa mwaka mmoja bondia Hassan Mwakinyo pamoja na kutozwa faini ya TZS milioni moja kwa kukiuka mkataba na kushindwa kupanda ulingoni.
Katibu Mkuu wa TPBRC, George Lukindo amesema sababu za Mwakinyo kushindwa kupanda ulingoni hazikuwa na mashiko na hivyo kukiuka kifungu cha 14 cha mkataba ambao umedhihirisha hatua za kufuatwa pindi bondia anapokwenda kinyume na mkataba.
“Msingi mkuu wa kutoa adhabu hiyo mi kwamba bondia Mwakinyo ni bondia mkubwa hapa nchini ambaye angepaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba anakuwa mfano bora kwa mabondia wengine wanaochipukia,” amesema.
Ameongeza kuwa “kitendo chake cha kujichukulia uamuzi pasipo kuheshimu mkataba hakika hakina afya kwa maslahi ya maendeleo ya michezo ya ngumi ya kulipwa Tanzania.”
Aidha, amesema Mwakinyo alionyesha tabia isiyoridhisha wakati akizungumza na kiongozi mkuu wa kamisheni ambapo alitoa maneno yasiyo ya hekima huku akieleza kuwa hakuna bondia aliyeko juu ya kamisheni inayoongozwa na kanuni na taratibu.
TPBRC imetoa siku saba kwa Mwakinyo kukata rufaa ikiwa hajaridhishwa na uamuzi huo.