Watatu wafariki, polisi ajeruhiwa kwenye vurugu za kutoa uchawi

0
52

Watu watatu wakazi wa Kijiji cha Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma wamethibitishwa kufariki katika vurugu zilizohusisha vitendo vya kutoa uchawi maarufu kwa jina la ‘Kamchape’.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amesema polisi wawili wamejeruhiwa katika vurugu hizo huku sababu za vifo vya wananchi hao bado hazijabainika.

Amesema vurugu zilianza baada ya polisi kufika kwenye Kijiji hicho kutoa elimu kuhusu madhara ya kukaribisha watu wanaotoa uchawi na kupiga marufuku kuendelea na vurugu hizo, lakini wananchi walikaidi agizo hilo na siku iliyofuata waliendelea na viendo vya kutoa uchawi kwenye nyumba za watu kwa kuwanyoa vipara wananchi ambao wanadaiwa uchawi umetolewa kwenye nyumba zao.

Kamanda ameongeza kuwa walifika kijijini hapo kuzuia vurugu hizo na wananchi hao walifunga Barabara Kuu ya Kigoma- Tabora inayopitia kijijini hapo kwa kuweka magogo na kuwasha moto ili kuzuia polisi na vyombo vya usalama wasifike kwenye maeneo wanayofanya matukio hayo, ndipo polisi walitoa vizuizi hivyo na kuanza kukamata watu, ambapo vurugu zilitokea na kupelekea vifo hivyo.

Aidha, amesema magari mawili ya polisi na uhamiaji yalivunjwa vioo na kituo cha polisi cha Kazuramimba kilishambuliwa kwa mawe.

Chanzo: Habari Leo

Send this to a friend