Wafungwa 691 wanasubiri adhabu ya kifo nchini

0
25

Wadau wa haki za binadamu wameitaka serikali kuondoa adhabu ya kifo na badala yake kuwe na sheria mbadala, wakieleza kuwa adhabu hiyo inakiuka misingi ya haki za binadamu.

Wakizungumza katika kongamano liliohusisha wadau kujadili adhabu hiyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia amesema mifumo ya haki nchini haipo madhubuti kiasi cha kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa anayehukumiwa kunyongwa kwa kosa la kuua ni kweli ana hatia.

“Adhabu hii ni hatarishi kwa uhai wa watu wasio na hatia, pia ni adhabu ambayo imepitwa na wakati kwa kuwa imejengwa katika mfumo wa kisasi kwamba anayeua na yeye auawe. Ukitengeneza mfumo wa haki kwa utaratibu huu hauwezi kubadili makosa ya mkosaji,” amesema.

Imeelezwa katika kongamano hilo kuwa, mara ya mwisho Tanzania kutekeleza adhabu ya kifo ni mwaka 1994, na hilo limepelekea mpaka sasa wafungwa 691 wanaotumikia adhabu hiyo kubaki wakiwa na sintofahamu juu ya hatma ya maisha yao.

Sheria ya kanuni ya adhabu, sura ya 16 imeainisha makosa yanayopelekea mtu kupewa adhabu ya kifo kuwa ni pamoja na mauaji ya makusudi na uhaini. Sheria hii ilitungwa 1945, na ilianza kufanya kazi Septemba 28, 1945.

Send this to a friend