Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajia kuwasilisha ombi la kurusha matangazo ya mechi zitakazochezwa katika mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2027 kwa lugha ya Kiswahili.
Akizungumza leo wakati akifanya ziara Ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), amesema Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda imefanikiwa kupata uwenyeji wa mashindano hayo mwaka 2027 ambayo ni fursa ya kutangaza lugha ya Kiswahili katika mashindano hayo.
“Tunataka Kiswahili kitengeneze fursa nyingi, mwaka wa fedha wa 2024/25 tutatenga fedha kwa ajili ya kukuza lugha hii ambayo kwa sasa imeajiri Watanzania 103 duniani, pamoja na kushirikiana na sekta binafsi katika kubidhaisha lugha yetu adhimu ya Kiswahili,” amesema Ndumbaro.
Utata waibuka baada ya Zimbabwe kupata miss ‘mzungu’
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema kipaumbele cha Serikali katika mwaka ujao wa fedha wa mwaka 2024/2025, ni kuhakikisha lugha ya Kiswahili inatoa ajira nyingi zaidi kwa Watanzania wengi duniani, kwa kuanza na Watanzania waishio nje ya nchi.
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kutaka lugha ya Kiswahili kiingie kwenye lugha tano kubwa zaidi duniani kutoka kwenye lugha kumi iliyopo kwa sasa.