Serikali yawarejesha nchini Watanzania waliokuwa Israel

0
23

Serikali imewarejesha nchini Watanzania tisa waliokuwa nchini Israel kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya Israel na kundi la Hamas na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kukosa makazi.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Watanzania hao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato amesema Serikali imefarijika kwa Watanzania hao kuitikia wito wa kuokoa maisha yao, na kwamba anaamini Watanzania waliobaki nchini humo busara zitawaongoza na kuamua kurejea nyumbani.

Ameongeza kuwa kurejea nyumbani kwa Watanzania hao kunatokana na utekelezaji wa uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kuwarejesha nyumbani raia wake waliokuwa nchini humo ili waendelee kuwa salama.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwashawishi Watanzania walioko nchini Israel ili waone haja ya kurudi nyumbani hadi pale hali ya machafuko itakapotengemaa nchini humo.

Naye mmoja wa Watanzania hao, Lucas Malaki ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo ya kuwarejesha nyumbani na kuongeza kuwa kitendo hicho ni cha upendo na cha kizalendo, huku wakiahidi kuwa raia wema nchini.

 

 

 

 

 

 

Send this to a friend