Rais Samia kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu Zambia
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Zambia kuanzia Oktoba 23 hadi Oktoba 25, mwaka huu ikiwa na lengo la kujenga ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika ziara yake nchini humo, Rais Samia amekubali pia mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 59 ya Uhuru wa Zambia, yatakayofanyika Oktoba 24, 2023, jijini Lusaka.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema maeneo ya kipaumbele katika ziara hiyo ni pamoja na namna bora ya kuboresha miundombinu inayounganisha Tanzania na Zambia ili kufikia faida za kiuchumi.
Aidha, ziara hiyo pia itaangazia namna ya kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Zambia pamoja na kuibua fursa mpya za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Ameeleza kuwa Rais atahudhuria kongamano la biashara kati ya Tanzania na Zambia, ambapo wafanyabiashara wakubwa 100 kutoka Tanzania watashiriki.
“Hii inaonyesha nia ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo na kuendeleza ushirikiano wa kikanda,” ameeleza Makamba.