Rais Samia na Rais wa Ujerumani wajadili yaliyotokea wakati wa ukoloni

0
25

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania iko tayari kufungua majadiliano na Ujerumani ili kujadili na kukabiliana na athari na mambo mbalimbali yaliyotokana na utawala wa Kijerumani nchini.

Ameyasema hayo Oktoba 31, 2023 wakati akimpokea Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier Ikulu jijini Dar es Salaam na kisha kuzungumza na waandishi wa habari ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku tatu iliyoanza Oktoba 30, mwaka huu.

“Najua kuna familia ambazo zinasubiri mabaki ya wapendwa wao ambao wako kule katika makumbusho mbalimbali za Ujerumani, yote hayo tunakwenda kuzungumza na kuona vipi twende nayo vizuri,” amesema Rais Samia.

Aidha, amesema katika mazungumzo na Rais Steinmeier wamesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kwa ajili ya manufaa ya nchi na watu wake, na kwamba ana imani kuwa ujio wake nchini utachangia katika kuimarisha zaidi ushirikiano hasa katika sekta za kibiashara na uchumi, ambao unazingatia misingi ya kuheshimiana na kuaminiana.

Naye Rais Frank-Walter Steinmeier amesema ana imani kuwa ziara yake nchini Tanzania italeta mafanikio mazuri kiuchumi na katika sekta mbalimbali huku asisitiza kuwa mahusiano baina ya Tanzania na Ujerumani yataendelea kuwepo kutokana na uaminifu uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Ujerumani ilianza kuitawala Tanganyika, sasa Tanzania, karne ya 19. Tanganyika ilianza kutawaliwa na Wajerumani baada ya Mkataba wa Berlin wa 1885, ambao uligawanya maeneo ya Afrika kati ya mataifa ya Ulaya.

Mnamo mwaka 1900 watu kadhaa wakiwemo machifu wa Kitanzania walinyongwa na wakoloni wa Kijerumani kisha vichwa na mafuvu yao yalitumwa Berlin na kuwekwa katika majumba ya maonesho ambayo yako huko mpaka sasa pamoja na vitu vingine ikiwemo mjusi mkubwa unaotumika kama maonesho ambao asili yake ni kutoka Tanzania.

Hata hivyo hivi karibuni, Serikali ya Ujerumani imesema iko tayari kushirikiana na Idara ya Makumbusho ya Taifa kumrejesha nchini mjusi huyo ambaye amekuwa akihifadhiwa katika nchi hiyo kwa muda mrefu.

Send this to a friend