Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier ameomba radhi juu ya mambo mabaya yaliyofanywa wakati wa utawala wa kikoloni wa Ujerumani nchini Tanganyika (sasa Tanzania), akieleza kuwa Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania ili kutathimini kwa pamoja yaliyopita.
Rais Steinmeier ametoa kauli hiyo leo Novemba 01, 2023 wakati alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji Songea mkoani Ruvuma inayoonesha historia katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.
“Ningependa kuomba radhi kwa kile ambacho Wajerumani walikifanya kwa mababu zenu hapa,” amesema na kuongeza kuwa “kilichotokea hapa ni historia inayotuhusu sisi na ninyi, historia ya mababu zenu na historia ya mababu zetu wa Ujerumani […] Nitazichukua simulizi hizi pamoja nami hadi Ujerumani, ili watu wengi zaidi katika nchi yangu wazijue.”
Rais Samia na Rais wa Ujerumani wajadili yaliyotokea wakati wa ukoloni
“Nataka kuwahakikishia kuwa sisi Wajerumani tutashirikiana nanyi kwa pamoja kutafuta majibu ya maswali ambayo hayajajibiwa, ambayo hayawapi amani,” ameeleza.
Inakadiriwa kati ya watu 200,000 hadi 300,000 kutoka jamii za makabila ya asili waliuawa kikatili, huku mashamba na vijiji vikiharibiwa na wanajeshi wa Ujerumani wakati wa vita vya Maji Maji.