Serikali: Elimu ya lazima itakuwa miaka 10 badala ya miaka saba ya sasa

0
24

Serikali imesema imefanya maboresho kwenye baadhi ya maeneo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ili kutoa elimu ya ujuzi badala ya elimu ya taaluma pekee ambapo elimu ya lazima itakuwa ya miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa.

Akitoa taarifa kuhusu maboresho hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa maboresho hayo utaanza mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba na badala yake kuanza kufanyika kwa tathmini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari.

Ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa kuhusu kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kwa changamoto mbalimbali zikiwemo, mfumo wa elimu kujikita zaidi kwenye elimu ya jumla na kukosa fursa za elimu na mafunzo kwa kuzingatia mahitaji na njia mbalimbali za ujifunzaji kutokidhi kulingana na mazingira.

TCCA yafafanua kuhusu kibali cha Helikopta ya CHADEMA

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni “mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu na upungufu wa nguvu kazi. Changamoto hizo zilizaa hitaji la kuboresha sera yetu ya elimu ili kukidhi mahitaji ya sasa na wakati ujao.”

Aidha, amesema elimu ya ualimu nayo itaanza kutolewa kwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita na kuendelea. “Mafunzo ya ualimu yatajumuisha mwaka mmoja wa mafunzo chini ya uangalizi (internship) baada ya kuhitimu mafunzo tarajali (Pre-service training).”

Amesema maeneo yaliyoboreshwa ni katika mfumo wa upimaji na tathimini ambao utazingatia mahiri zinazohitajika kwa kila ngazi kwa lengo la kuwa na upimaji endelevu na matumizi ya mbinu mbalimbali za upimaji na tathmini ya maendeleo ya wanafunzi katika kujifunza.

“Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu ya msingi na Sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana pia Serikali itaweka utaratibu wa kubaini na kuendeleza wanafunzi wenye vipaji na vipawa mbalimbali,” ameeleza.

Send this to a friend