Baada ya kipande cha video kinachowaonesha watoto wa shule za msingi wakicheza wimbo wa msanii Zuchu ‘Honey’ wilayani Tunduma kusambaa mitandaoni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameagiza walimu wakuu wawili wa shule hizo wavuliwe vyeo.
Amesema hayo nje ya Bunge jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu video hiyo ambapo pia amepiga marufuku wanafunzi kucheza nyimbo zisizo na maadili na kuwataka walimu kuwa wasimamizi wa maadili pindi wanafunzi wawapo shuleni.
“Tumeshatambua shule yenyewe iko Tunduma, kulikuwa na kikundi kimeenda kutoa msaada shuleni pale, baada ya kutoa msaada ule kikaweka na muziki halafu wanafunzi wakacheza, na maudhui ya muziki wenyewe kila mtu ameusikia sina haja ya kuurudia,” amesema Profesa Mkenda.
Ameongeza, “tumeongea na wadhibiti ubora wapeleke taarifa kule, mkurugenzi awaondoe walimu wakuu wa shule mbili; moja shule ya Tunduma na nyingine ambazo ni kama shule pacha, waondolewe madaraka ya ukuu wa shule watafutwe wakuu wengine wa shule. Tunafanya hivi ili kutuma ujumbe, walimu wakuu tusaidieni msiruhusu vitu kama hivi viingie mashuleni.”
Serikali: Elimu ya lazima itakuwa miaka 10 badala ya miaka saba ya sasa
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza Profesa Mkenda kwa kukemea kitendo hicho na kutoa wito kwa watoa huduma wote na wanaohudumia watoto kusimamia malezi na makuzi ya watoto.