Tamko la Wizara ya Afya ufaulu wa mitihani ya madaktari watarajali

0
11

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amelielekeza Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) kuendelea kuendesha mitihani yote ya kabla ya utarajali (pre- internship examination) na baada ya utarajali (post internship examination) kabla ya kutoa leseni ya kutoa huduma za tiba kwa mwanataaluma husika.

Hayo yameelezwa katika taarifa ya wizara iliyotolewa kwa vyombo vya habari juu ya matokeo ya uchunguzi wa kamati huru kuhusu ufaulu wa mitihani ya madaktari watarajali (Intern Doctors) inayoendeshwa na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT).

Aidha, Waziri amemwagiza mganga mkuu wa serikali kufanya tathmini ya kina ya mafunzo ya watarajali katika hospitali mbalimbali za umma na binafsi nchini zinazopokea watarajali na kuwasilisha mapendekezo ya kuimarisha ubora wa mafunzo na usimamizi wao.

Mbali na hayo, amemwagiza katibu mkuu wizara ya afya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na wizara ya elimu, vyuo vinavyotoa mafunzo ya fani za afya na taasisi za ithibati ili kuboresha mafunzo kwa upande wa madaktari na kada nyingine za sekta ya afya.