Waziri amsimamisha kazi Mkurugenzi akiwa bungeni

0
28

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ametoa ujumbe kwa viongozi wazembe na wabadhirifu katika wizara yake kwamba siku zao zinahesabika.

Akizungumza bungeni wakati akichangia taarifa ya kamati za bunge kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amesema Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi kubwa, hivyo ni lazima viongozi waende sambamba na kasi ya Rais Samia Suluhu kwa kufanya kazi kwa bidii ili kushinda kwa urahisi uchaguzi wa mwaka 204 pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Wale wote ambao wametajwa kwenye ripoti, naomba niseme maneno yafuatayo, ole wake kiongozi yeyote mzembe na mbadhirifu. Kiongozi yeyote mzembe kwenye wizara yangu na asiye na nidhamu nitakayemkuta huko na wabadhirifu, nataka niwaambie siku zao zinahesabika,” amesema Mchengerwa.

Aidha, amemwelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kumsimamisha kazi mara moja Mkurugenzi wa Igunga, Athuman Msabila kutokana na ushiriki wake katika fedha za mifumo kwa kushirikiana na watendaji wawili wa mifumo walioko TAMISEMI ambao walitajwa katika taarifa ya ripoti.

“Tutahakikisha tunawatendea haki Watanzania, Serikali inafanya kazi kubwa sana. Ni lazima tumtendee haki Mheshimiwa Rais na sisi viongozi kufanya kazi kwa bidii, hakuna lugha nyingine,” ameeleza.

Mchengerwa ameongeza taarifa za CAG na LAAC zinawakumbusha viongozi kufanya kazi na kurekebisha pale walipoanguka ili kuleta maendeleo yaliyokusudiwa.

Send this to a friend