EWURA yabadili utaratibu kwa waagizaji mafuta
EWURA yabadili utaratibu kwa waagizaji mafuta
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema ili kuongeza ushindani zaidi katika uagizaji wa mafuta nchini, kampuni yoyote iliyopewa leseni ambayo haitoagiza mafuta ndani ya miezi mitatu, leseni yake itakufa.
Mkurugenzi wa EWURA, Dkt. James Andilile amesema hayo wakati wa mkutano na vyombo vya habari, ambapo pia amesisitiza kuwa kampuni itakayoagiza mafuta itahitajika kuagiza kwa uwiano wa soko lake (market share).
“Kabla ya mwezi huu kampuni zilizopewa leseni za kuagiza mafuta, leseni zao zilikuwa zinabaki hai ikiwa wameagiza mafuta mara moja tu ndani ya miezi sita, kwahiyo unakuta tuna makampuni mengi lakini hayafanyi kazi kwa sababu anajua ikikaribia kufa leseni nitaagiza mara moja kisha itaendelea kuwepo.
Kwahiyo tumebadilisha, tumeboresha kanuni, kwa kushirikiana na wadau ambapo sasa kampuni ambayo haitaagiza mafuta ndani ya kipindi cha miezi mitatu leseni yake itabidi ife,” amesema.
Aidha, Dkt. Andilile ameweka wazi kuwa upangaji wa bei za mafuta nchini unaathiriwa na mambo mbalimbali ikiwemo kushuka kwa thamani ya fedha, bei za uletaji mafuta, mwenendo wa bei kwenye soko la dunia, kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
Mbali na hayo, amesema ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme, Serikali imejielekeza kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo maji na nishati jadidifu hususani katika masuala ya joto ardhi, umeme jua pamoja na umeme kwa njia ya upepo.