Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano leo Dar es Salaam

0
29

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanyika leo kutokea misikiti mbalimbali kuelekea katika maeneo ya Manzese, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Muliro amesema kwa yeyote atakayekiuka onyo hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawatahadharisha wananchi kuhusu taarifa zinazosambaa mitandaoni kutoka kwa mtu mmoja anayedai kuwa leo, Novemba 10, 2023, kutakuwa na maandamano yatakayotokea kwenye misikiti mbalimbali kuelekea maeneo ya Manzese,” amesema.

Wanaotengeneza biskuti zenye bangi wakamatwa Dar es Salaam

Amesisitiza kwamba mtu huyo ambaye jina lake halikuwekwa hadharani alipaswa kupeleka taarifa yake kituo cha polisi, lakini badala yake ameendelea kuhamasisha watu kuingia mitaani na kufanya maandamano.

“Polisi Dar es Salaam inaendelea kuwatahadharisha watu kutoshiriki maandamano hayo kwa sababu yapo kinyume na sheria. Na wasiingie barabarani na kuzuia shughuli mbalimbali za kiuchumi za watu ambazo zipo kwa mujibu wa sheria. Kufanya hivyo itakuwa ni sehemu ya makosa kwa kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku,” ameongeza.

Send this to a friend