Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameagiza kuondolewa kwa Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana na kushindwa kutoa taarifa mbalimbali na kutofanya mikutano na wananchi wanaozunguka miradi ya gesi asilia, ikiwemo dharura zinazotokea katika Mkuza wa Bomba la Gesi.
Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo wakati aliposimama katika Kijiji cha Msimbati wilayani Mtwara ili kuzungumza na wananchi akiwa anatokea kukagua visima vya kuzalisha na mitambo ya kuchakata gesi ya Mnazi Bay iliyopo katika Kata ya Msimbati.
Wananchi walimweleza Dkt. Biteko kuhusu changamoto walizonazo ikiwemo barabara, kituo cha afya, kutopata fedha zozote kutokana na kazi za uzalishaji wa uchakataji gesi asilia unaofanyika kwenye kijiji hicho na kutopata taarifa mbalimbali za mradi ikiwemo zinapotokea changamoto kwenye bomba la gesi asilia.
Katika hatua nyingine, ameagiza Meneja wa Huduma kwa Wateja katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuondolewa katika nafasi hiyo kutokana na majibu yasiyostahiki wanayojibiwa wananchi wanapopiga simu kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Dkt. Biteko amesema miradi inapotekelezwa katika eneo lazima ibadilishe maisha ya wananchi, ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile shule, vituo vya afya, barabara na maji.