Biteko aiagiza TANESCO kuzikatia umeme taasisi za Serikali inazozidai

0
15

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata umeme kwa wadaiwa wote wasiolipa gharama za kutumia umeme ambapo shirika hilo linadai shilingi bilioni 224 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, hali inayopelekea changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.

Amesema hayo Novemba 26, 2023 wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipokagua kituo cha umeme cha Lemuguru mkoani Arusha ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya ( Kenya- Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP)).

“Hapa Arusha tu, TANESCO anadai wateja wake shilingi bilioni 7.7, na mara nyingi wanaodaiwa si wananchi wadogo wadogo bali taasisi za Serikali na wawekezaji wanaojiita wawekezaji wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira, TANESCO inahitaji fedha ili awekeze na kisha awapelekee umeme wananchi, TANESCO nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai ili mradi unamdai kwa haki,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe. “Huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha Huduma kwa Mteja tukiimarishe kutoka miito 65 na ziongezwe kufika 100 na zaidi.”

Send this to a friend