Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali ipo kazini kuhakikisha suala la kukatika kwa umeme linashughulikiwa kikamilifu na hakuna hujuma yeyote kama ambavyo inasemekana.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la mwananchi wa Kijiji cha Masimba, Kata ya Tongwe wilayani Muheza kuhusu kukatika kwa umeme kijijini hapo.
“Niwahakikishie ndugu zangu, Mheshimiwa Rais alitupa miezi sita kuhakikisha tunaondoa mgao wa umeme, tupo kazini na kwa mipango ambayo tunayo tunategemea ndani ya miezi sita hiyo tutakuwa tumeshaondoa mgao wa umeme.
Miezi sita inaisha mwezi wa tatu 2024, mpaka kufikia hapo na kwa mipango iliyopo miradi ambayo Mheshimiwa Rais ametupatia fedha tunatekeleza tunategemea tutaondoka kabisa kwenye mgao wa umeme.”
Katibu Mkuu CWT aliyegoma kurudi kufundisha asimamishwa kazi
Ameongeza kuwa “Kwa kipindi hiki mvua zinanyesha, maeneo kwa maeneo, maeneo ambayo tunafanya uzalishaji wa umeme kule kwenye mabwawa yetu ya umeme Kidatu, Kihansu na Mtera ndio mvua zimeanza kwa hiyo tunategemea kadiri mvua zinavyoendelea kunyesha, maji yanavyoendelea kujaa tutakuwa tumepunguza tatizo kwa kiasi kikubwa.”
Aidha, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inatoa huduma bora na stahiki ya upatikanaji wa umeme ambao ni wa kudumu na utawasaidia wananchi kwenye shughuli za maendeleo.