Mambo 4 ya kuzingatia unapoomba kuongezwa mshahara kazini

0
85

Kuongea na mwajiri juu ya kuboreshewa maslahi yako kazini inaweza kuwa suala gumu ambalo linaambatana na uoga wa kukataliwa uliopo kwa waajiriwa wengi, hivyo linahitaji ujasiri na maarifa ambayo yatakusaidia kufanikisha jambo hilo.

Hata hivyo kampuni nyingi huboresha maslahi ya wafanyakazi wake ikiwemo kuongeza mishahara kila baada ya kipindi fulani, lakini baadhi hazifanyi hivyo.

Ili kuwasilisha ombi la maboresho ya maslahi yako unapaswa kuzingatia mambo haya yafuatayo;

Tambua Thamani Yako
Jua ni kwa jinsi gani unavyochangia kwenye kampuni au shirika lako. Ikiwa unaweza kuonyesha jinsi kazi yako inavyosaidia malengo ya kampuni, unaweza kuwa na msingi imara wa kujadili maslahi yako.

Zingatia muda
Ingawa ni kawaida kuomba ongezeko la mshahara kila mwaka, inatakiwa pia uwe makini kwenye kupangilia ni muda gani hasa uombe ongezeko hilo. Angalia pia hali ya kiuchumi ya kampuni kwa wakati husika unaotaka kutuma ombi hilo.

Onyesha ujuzi wako
Ni lazima uoneshe ni kwanini unataka au unastahili kuongezewa mshahara. Pitia kazi zote ulizofanya kwa mwaka ulioisha na uangalie ulizomaliza kikamilifu na jinsi gani zimechangia kwenye malengo ya biashara.

Ongea na mwajiri wako
Kama umefanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja, basi utakuwa unajua ni njia gani nzuri zaidi ya kumfuata mwajiri wako ili kuzungumza kuhusu ongezeko la mshahara. Weka wazi malengo yako, ongelea utendaji wako na jinsi unavyochangia katika shirika.

Kumbuka, kama unafanya kazi kwa bidii na unachangia katika maendeleo ya kampuni hupaswi kuwa na woga wa kufanya mazungumzo kuhusu jambo hili bali zingatia wasilisho lako kufanyika kwa heshima na kwa muktadha unaofaa.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend