Rais Samia Suluhu Hassan amesema Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) linapaswa kuzingatia udhibiti wa mitihani katika utungaji na usahihishaji ili kuzalisha nguvu kazi yenye tija kwa taifa.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya NECTA mkoani Dar es Salaam, amesema wahitimu wengi wanashindwa kufanya kazi zao ipasavyo pindi wanapoajiriwa kutokana na kutokuwa na sifa stahiki.
“Tukitoa mianya ya watoto wetu kufanya mitihani kwa kuijua kabla au kupenyeza mitihani, tunatoa product ambayo haikupikwa vizuri, haikuiva kwenye kichwa, pamoja na kwamba kutoka darasani si kuweza kufanya kazi mbalimbali wanazoajiriwa,” amesema.
Rais Samia: Tuendelee kudumisha amani yetu kwa mustakabali wa taifa
Aidha, amesema pamoja na kazi iliyofanywa na Serikali ya kuhakikisha inaboresha miundombinu bora ya elimu, bado juhudi kubwa zinahitajika kutokana na idadi kubwa ya watu inayoendelea kukua kila mwaka.
“Ongezeko hili la wanafunzi linachangiwa pia na sera ya msisitizo wa Serikali kuhakikisha kila mtoto nchini anapata fursa ya elimu, na hili ni agizo kwenye dira yetu ya miaka 25” ameeleza.
Mbali na hayo, amesema Serikali itaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu ili kuhakikisha ufundishaji, usomeshaji na utahini unafanyika kwa umahiri mkubwa kuwezesha watahiniwa kumudu mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.