Hedhi hutokea kila mwezi kama sehemu ya mzunguko wa kawaida wa kibaiolojia wa mwanamke. Kwa kawaida hudumu kwa siku 3 hadi 7, ingawa inaweza kutofautiana kati ya wanawake.
Baadhi ya wanawake wameripotiwa kutumia vitu vya asili kama limao au dawa aina ya flagly kukatisha hedhi, jambo ambalo linaelezwa na madaktari kuwa ni hatari kwa afya zao.
Kwa mujibu wa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka jijini Dar es Salaam, Isaya Mhando amesema wanaotumia ndimu au limao vinaweza kusababisha kuharibu kinga inayozuia bakteria waharibifu na fangasi ili wasiingie ndani.
Mbeya yafunga mashine za ATM za kujipima UKIMWI
“Kwa kufanya hivyo unaharibu mazingira ya wale bakteria na kinga ya mazingira ya uke inapotea, ndiyo sababu kuna wengine wanatoka uchafu na wapo wengine hata kama hawatoki uchafu lakini uke unatoa harufu kali mithiri ya shombo la samaki,” ameeleza.
Ameongeza kuwa, “hakuna sayansi ya kuzuia hedhi kwa ndimu au limao na hata wanaodai kutumia flagly, swali la kujiuliza ni dawa hiyo hutibu nini na wewe umemeza ili kutibu nini?”
Naye daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama katika hospitali ya Morogoro, Daniel Nkungu ameeleza kuwa njia hizo zinazotumiwa kukatisha hedhi zinaweza kuathiri mfumo wa uzazi na hivyo kupelekea kushindwa kubeba ujauzito kwani vitu hivyo huweza kupanda na kwenda kwenye mayai.
Chanzo: Mwananchi