Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema hali inayoendelea kwa sasa kwa baadhi ya wateja kulalamika mita za LUKU kutumia umeme zaidi tofauti na matumizi yao kwa miezi ya nyuma, haitokani na ubora wa LUKU isipokuwa sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la matumizi ya umeme yaliyochangiwa na wengi kuwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Katika taarifa iliyotolewa na TANESCO imesema katika miezi ya Desemba na Januari matumizi ya umeme majumbani huwa ni makubwa ukilinganisha na miezi mingine kutokana na watu wengi kuwa majumbani na kupelekea matumizi mengi ya vifaa vya umeme.
“Vilevile mabadiliko ya hali ya hewa yanayopelekea kuwa na ongezeko kubwa sana la joto na hivyo kupelekea wakazi wengi kutumia vipoozeo na hivyo kuongeza kiwango cha matumizi ya umeme,” imesema.
Imeongeza kuwa “mita za LUKU zinazopima matumizi ya umeme kwa wateja zina ubora wa hali ya juu unaokubalika kwa viwango vya kimataifa vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Hata hivyo, ili kuthibitisha ubora na usahihi wa mita, shirika linafanya uhakiki wa mita kabla ya mita hizo hazijatumika kwa wateja ili kujiridhisha na viwango vya ubora.”
Aidha, TANESCO imewahimiza wateja wake kutumia vifaa vya umeme pale vinapohitajika pamoja na kufanya ukaguzi wa mtandao wa nyaya za umeme ndani ya majengo angalau mara moja kila baada ya miaka mitano.