Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuanza kufanya maandamano ya amani ya kushinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi, ikiwemo maboresho ya Katiba ili kuwezesha kupata tume huru ya uchaguzi.
Akizungumza leo na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema Serikali imepuuza maoni yaliyotolewa na Kikosi Kazi pamoja na wadau mbalimbali, hivyo chama hicho kimeamua kufanya maanadamano ya amani yatakayoanza Januari 24 mkoani Dar es Salaam na kuendelea mpaka serikali itakapoondoa bungeni miswada ya maboresho ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa.
“Tanzania ni yetu sote na hatuna budi kuilinda na kuipigania kesho yetu na kesho ya watoto wetu iliyo bora zaidi. Sisi kama kizazi tutakapokosa ujasiri wa kusimama na kusema basi imetosha, tutajenga taifa la watu waoga na taifa la watu wasio na ujasiri,” amesema.
Burundi yafunga mipaka yake na Rwanda
Kwa upande wa kupanda kwa gharama za maisha, Kamati Kuu imeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kupunguza tozo na kodi kwenye bidhaa na huduma muhimu kwa wananchi pamoja na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima Serikalini ili kuokoa mapato.
Kadhalika, imeitaka Serikali kutengeneza mpango na mkakati mahususi wa kuwakwamua wananchi na hali ngumu ya maisha ikiwa ni pamoja na kushusha bei ya bidhaa muhimu na kuweka ruzuku kwenye baadhi ya bidhaa ili wananchi wafurahie maisha yao.
“Tunataka Serikali ijue this time around we are very serious. Kuanzia sasa viongozi wa mikoa, viongozi wa majimbo, viongozi wa kata, viongozi wa mitaa tunataka maandalizi yafanyike katika kona zote za Dar es Salaam. Tutaratibu jambo hili kuanzia sekretarieti ya taifa kwa kushirikiana na uongozi wa kanda na ngazi zote za kiuchaguzi ndani ya chama chetu,” ameeleza.