Benki Kuu yatangaza riba elekezi kwa mikopo ya benki

0
34

Kamati ya Sera ya Fedha imetangaza Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia 5.5 kwa robo ya kwanza ya mwaka huu ili kutimiza malengo ya kiuchumi katika kipindi hicho, ikielezwa kuwa imezingatia lengo la kuhakikisha thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni inaendelea kuwa imara.

Katika taarifa iliyotolewa na benki hiyo imesema kiwango cha Riba ya Benki Kuu kilichotangazwa kinaendana na malengo ya kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabakia ndani ya lengo la asilimia 5 na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia lengo la asilimia 5.5 au zaidi kwa mwaka 2024.

Gavana wa Benki Kuu na Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Emmanuel Tutuba amesema ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo hayo, Benki Kuu itatumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha kuhakikisha riba katika soko la fedha baina ya benki nchini inakuwa tulivu.

“Benki Kuu itakuwa inafuatilia mwenendo wa riba ya mikopo ya siku 7 katika soko hilo na kuchukua hatua kuhakikisha mabadiliko ya riba yanakuwa ndani ya wigo usiozidi asilimia 2 chini au juu (+/-2%) ya Riba ya Benki Kuu, amesema.

Mfumo wa kutumia riba unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Sera ya Fedha. Aidha, mabadiliko hayo yanaelezwa kuendana na makubaliano ya Itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa ni mojawapo ya hatua kuelekea kuwa na sarafu moja na Benki Kuu moja ya Afrika Mashariki.

Send this to a friend