Benki ya NMB yapata mafanikio ya kihistoria; yatengeneza faida ya TZS bilioni 775 kabla ya kod
- Faida kabla ya kodi: Shilingi Bilioni 775, ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka
- Faida baada ya kodi: Shilingi Bilioni 542, ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka
- Jumla ya Mapato: Shilingi Trilioni 1.4, ongezeko la asilimia 18 kwa mwaka
- Jumla ya Mali: Shilingi Trilioni 12.2, ongezeko la asilimia 19 kwa mwaka
- Bei ya Hisa za NMB: Ongezeko la asilimia 49 kwa mwaka
Rekodi hii ya faida imetokana na ukuaji mkubwa wa mikopo, kuogezeka kwa wateja na miamala, kuongezeka kwa amana za wateja, ubora wa mikopo na kiwango cha juu cha ufanisi.
Dar es Salaam, Januari 30, 2024. Benki ya NMB imevunja rekodi nyingine kiutendaji kwa mwaka 2023, baada ya kutengeneza faida kabla ya kodi ya Shs Billion 775, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji makini wa mkakati wa Benki.
Jumla ya mapato ya Benki yamefikia Shilingi Trilioni 1.4 yanayotokana na ukuaji wa asilimia 24 wa mapato ya riba na asilimia 15 ya mapato yasiyotokana na riba (NFI). Ongezeko la mapato ya riba lilitokana na ukuaji mkubwa (asilimia 28 kwa mwaka) wa mikopo, huku ongezeko endelevu la wateja, shughuli za kuwahudumia wateja na ongezeko la miamala vikipelekea ukuaji wa mapato yasiyotokana na riba.
Benki pia iliendelea kuonyesha ufanisi mkubwa kwenye gharama za uendeshaji na ubora wa mikopo. Uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato uliboreshwa zaidi hadi kufikia asilimia 39, wakati uwiano wa mikopo chechefu umeshuka hadi kufikia asilimia 3.2. Takwimu hizi zote ni chini ya ukomo wa kikanuni wa Benki Kuu wa asilimia 55 na asilimia 5.
Kutokana na ufanisi huu, faida kabla ya kodi imeongezeka kwa asilimia 26 hadi Shilingi Bilioni 775 huku Faida baada ya Kodi ikifika Shilingi Bilioni 542 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka. Hiki ni kiwango kikubwa cha faida na cha kihistoria kwa benki ya NMB na sekta nzima ya fedha nchini.
Mizania ya Benki imeendelea kukua na kufikia jumla ya mali ya Shilingi Trilioni 12.2 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 19 kwa mwaka, huku ukwasi na mtaji wa Benki ukiwa imara na juu ya viwango vya Benki kuu. Ukuaji huu ulitokana hasa na kukua kwa amana za wateja kwa asilimia 11, pamoja na ongezeko la mikopo la asilimia 28. Hadi kufikia Disemba 2023, mtaji mkuu wa Benki ulikuwa asilimia 20.17.
Akizungumzia matokeo hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema:
“Tunajivunia ufanisi mkubwa na matokeo chanya ya kiutendaji yaliyopatikana katika maeneo muhimu ya utekelezaji wa Mkakati wetu, ikiwemo ujumuishwaji wa watanzania kwenye sekta rasmi ya kifedha, utoaji wa huduma bora kwa wateja, na uwekezaji wa kimkakati kwa wafanyakazi wetu, utawala bora na uwekezaji kwenye teknolojia ili kuongeza thamani.”
Utekelezaji wa mkakati wetu umetuletea matokeo chanya na hatua muhimu:
- Mwaka 2023 tumeweza kufungua akaunti mpya za wateja zaidi ya milioni 1.2, na kufanya jumla ya akaunti za wateja wetu kufikia zaidi ya akaunti milioni 7.1
- Tuliongeza kasi ya uwekezaji kwa wafanyakazi wetu inayotufanya kuwa Mwajiri Pendwa. Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kiliitaja Benki ya NMB kama Mwajiri Bora wa Mwaka 2022 na mshindi wa jumla wa pili mwaka jana (2023).
- Tumeendelea kuwa kinara wa uwekezaji na ubunifu wa kidijitali, huku uwekezaji wetu katika eneo hili ukizidi kutambulika kimataifa. Majarida ya kimataifa ya The Euromoney, Global Business, na International Bankers yote yametutaja kuwa “Benki Bora kwa Masuluhisho ya Kidijitali na Kibunifu”.
Dhamira ya kujitolea kusaida jamii na kuhifadhi mazingira ilionekana dhahiri. Mwaka 2023, tuliwekeza zaidi ya TZS bilioni 6 kwenye elimu, afya na mazingira. Aidha, tuliendelea na jukumu la kutekeleza ajenda ya uendelevu kwa kuweka sokoni hatifungani ya masuala ya maendeleo endelevu iliyofikisha mauzo ya shilingi Bilioni 400. Katika kutambua hilo, tumetajwa kuwa Benki Bora ya Uwajibikaji kwa Jamii – CSR (Euromoney), na Benki Bora kwa Mazingira na Utawala Bora Kibiashara – ESG (the International Banker).
- Uendeshaji biashara kwa uadilifu na misingi ya utawala bora kunaendelea kutufanya tuwe tofauti. Mwaka 2023 Jarida la Global Business & Finance, limeitaja NMB kama “Benki Salama Tanzania”, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikitutaja kama Mlipa Kodi Mkubwa Zaidi Tanzania na Mlipa Kodi Bora anayelipa Kodi kwa kuzingatia sheria za kodi nchini.
Mafanikio haya bila shaka yanaendelea kuionyesha NMB kama Benki kiongozi nchini Tanzania. Jarida la Euromoney kwa mara nyingine tena, ikiwa ni mara ya kumi katika miaka 11 limeitaja Benki ya NMB kama Benki Bora zaidi Tanzania, na hivyo kuzidi kuonyesha ukubwa na nafasi ya Benki ya NMB nchini.
Ufanisi na matokeo haya ya kiutendaji vimekuwa na matokeo chanya hata kwenye bei ya hisa za NMB na ukubwa wa mtaji katika soko la hisa na hivyo kuleta matumaini makubwa kwa wanahisa wake. Tangu Januari 2023, bei ya hisa za NMB iliongezeka kwa asilimia 49 kutoka shilingi 3,020 hadi kufikia shilingi 4,500 mwishoni mwa Disemba 2023 (bei ya juu kabisa kufikiwa mwaka wa 2023 ilikuwa shilingi 4,880).
Ongezeko hili la bei ya hisa limefanya mtaji wa Benki ya NMB kwenye soko la hisa kufikia shilingi Trilioni 2.25 hadi Disemba 2023 kutoka shilingi Trilioni 1.5 za Disemba 2022, na kufanya NMB kuwa:
- Benki kubwa zaidi iliyoorodheshwa kwenye soko la hisa Tanzania na masoko yote ya hisa Afrika Mashariki (Thamani ya kampuni kwenye soko la hisa yaani market capitalization)
- Kampuni ya nne kwa ukubwa kwa Kampuni zilizoorodheshwa Afrika Mashariki, baada ya Safaricom, TBL, na MTN-Uganda,
- Kampuni ya 26 kwa ukubwa kati ya kampuni zilizoorodheshwa Kusini mwa Jangwa la Sahara (ukiondoa Afrika Kusini), hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa NMB kuwa katika orodha hiyo, na kuwa benki pekee ya Tanzania kuwahi kuingia kwenye orodha ya kampuni 30 kubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara (ukiondoa Afrika Kusini).
“Mafanikio yaliyopatikana mwaka 2023 yanaonyesha jukumu la NMB kuendelea kuwa injini ya ustawi wa kiuchumi nchini, na mwezeshaji wa kuzifungua fursa mpya kwa wateja na wadau wetu wote Tanzania. Hakika huu ni ushahidi na heshima wanayutupa wateja wetu, imani waliyonayo wanahisa kwetu, na kujitolea kwa wafanyakazi wetu, ambao wameendelea kuwa chachu ya hatua hizi muhimu na za kihistoria,” Bi Ruth aliongeza.
Shukurani kwa matokeo haya ya mwaka wa fedha wa 2023 na hatua zote muhimu za kimkakati zilizopigwa ni maalum kwa wateja wetu, washirika wote wa Benki, na Watanzania wote kwa mchango wao thabiti na imani waliyonayo kwa Benki ya NMB. Aidha, tunaishukuru Serikali yetu kupitia Benki Kuu ya Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi yanayozingatia ubunifu na kuchochea ukuaji endelevu.