Tanzania yasajili miradi ya uwekezaji trilioni 4 kwa miezi mitatu

0
27

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu ya mwisho wa mwaka 2023, kimesajili miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.4 [takribani TZS trilioni 4].

TIC imesema hiyo ni ongezeko la asilimia 80 kulinganisha na miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 769.6 [takribani TZS trilioni 2] iliyosajiliwa kwenye kipindi kama hicho kilichopita (Oktoba-Desemba 2022).

“Ongezeko hilo kubwa la uwekezaji limetokana na ziara za nje za Rais Samia Suluhu Hassan za kuvutia wawekezaji kupitia diplomasia ya uchumi na kuimarishwa kwa mazingira ya biashara nchini ambayo yamevutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani,” imesema taarifa ya TIC.

Aidha, Sekta tano zilizotajwa kuongoza kwenye uwekezaji huo ni viwanda Dola milioni 690.8 [TZS trilioni 1.7] usafirishaji Dola milioni 241.8 [TZS bilioni 610.5] huduma Dola milioni 122.5 [TZS bilioni 309.3], kilimo Dola milioni 89.1[TZS bilioni 224.9] na utalii Dola milioni 83.3 [TZS bilioni 210.3] ambapo miradi iliyosajiliwa Oktoba hadi Desemba 2023 inatarajiwa kutengeneza jumla ya ajira mpya 18,390, kutoka ajira 10,216 za kipindi kama hicho kilichopita kwa mwaka 2022.

Kwa mujibu wa takwimu za TIC, mikoa ya Dar es Salaam na Pwani imeongoza kwa kupata uwekezaji mkubwa zaidi nchini kwenye miezi mitatu ya mwisho wa mwaka jana ambapo Dar es Salaam iliweza kuvutia miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 454.7 [TZS trilioni 1.1], wakati mkoa wa Pwani ulipata miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 380.7 [TZS bilioni 961.2].

Send this to a friend