Safari ya Edward Ngoyai Lowassa duniani umefikia mwisho Februari 10, 2024, ambapo ameacha simulizi mbalimbali kwenye siasa na maeneo mengine aliyohudumu enzi za uhai wake.
Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli akiwa mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa na kuanza masomo yake katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.
Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha Kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 – 1971, na kisha kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora.
Alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974 hadi mwaka 1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo.
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa afisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977 hadi mwaka 1989.
Lowassa aliwahi pia kutumikia jeshi la Tanzania na hata kupigana katika vita kati ya Tanzania na Uganda vilivyopelekea Idd Amin kuondolewa madarakani.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC) mwaka 1989 hadi mwaka 1990.
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia kundi la vijana ndani ya CCM na akashikilia nafasi hiyo kati ya mwaka 1990 hadi 1995 na mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri.
Kwenye uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3 na alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili kisha mwaka 1997 hadi mwaka 2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu na ndipo Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mfugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
Mwaka 2005, Lowassa aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na akahudumu katika nafasi hiyo hadi Februari 2008, baada ya kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond.
Baada ya kujiuzulu, aliendelea kushiriki katika siasa, ambapo aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote.
Mwaka 2015, Lowassa alitangaza nia yake ya kugombea urais kupitia CCM. Hata hivyo, baada ya kutoelewana na chama chake, alitangaza kujiondoa na kujiunga na chama cha upinzani, CHADEMA, miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu na kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CHADEMA.
Kila kona aliyozunguka, mikutano yake ya hadhara ilivutia maelfu ya watu waliomuunga mkono japokuwa hakufanikiwa kushinda nafasi hiyo.
Baada ya miaka minne tangu alipohamia upinzani mwaka 2019 Lowassa alitanganza kurudi CCM na kukaribishwa rasmi na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli katika ofisi ndogo za CCM jijini Dar es salaam.
Moja kati ya jitihada kubwa alizofanya wakati akiwa waziri mkuu ni pamoja na kufanikisha upatikanaji wa fedha za kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma.
Lowassa ameanza kuugua tangu Januari 14, 2022 na kupata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na baadaye kupelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi na kisha kurejea tena katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambapo ndipo alifikwa na umauti Februari 10, 2024.
Lowassa ameacha mke na watoto watano.