Akamatwa kwa kuiba mtoto ili awaridhishe wakwe zake

0
15

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Mariam Renatus (22) kwa tuhuma za kuiba mtoto wa miezi 10, Miracle Ayoub eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam na kwenda naye hadi Kijiji cha Bugalama mkoani Geita.

Awali jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kuibwa kwa mtoto huyo Februari 6 mwaka huu majira ya saa 1 usiku kutoka kwa mama wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Victoria Charles (34) mkazi wa Gongo la Mboto ambapo mtuhumiwa alijifanya msaidizi wa ndani na kumuiba mtoto huyo.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mtuhumiwa alimuiba mtoto huyo kwa lengo la kuwaridhisha familia ya wakwe zake baada ya kuwadanganya kuwa alijifungua mtoto tangu Mei 2023 ambaye alizaa na kijana wao.

“Mtoto amepatikana akiwa na afya njema na mtuhumiwa atafikishwa haraka iwezekanavyo mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili,” imesema taarifa ya polisi.

Hata hivyo jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa makini na vijana wa kike wanaojifanya wanatafuta kazi za ndani na baadaye kuwaibia.

Send this to a friend