Waziri Mkuu wa Ethiopia kufanya ziara ya kitaifa ya siku tatu Tanzania

0
27

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Dkt. Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia Februari 29 hadi Machi 2 mwaka huu kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) imeeleza nia ya ziara hiyo ni kudumisha na kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Ethiopia huku ikijikita zaidi katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ushirikiano kwenye usafiri wa anga.

“Tumeona manufaa makubwa ya ushirikiano huo kwa sababu katika miaka sita iliyopita, marubani 75 wa Tanzania wamepata mafunzo nchini Ethiopia na wahandisi wa ndege 23 pia wamepata mafunzo nchini Ethiopia. Tunaamini ziara hii itawezesha kufungua milango zaidi kwa marubani wengi zaidi na wahandisi wa ndege wengi zaidi kujifunza masuala hayo nchini Ethiopia,” amesema Makamba.

Dkt. Mpango: Serikali inatarajia kupokea ndege mpya mbili

Ameongeza kuwa ziara hiyo pia italeta fursa katika maeneo mbalimbali ikiwemo mifugo, ulinzi na usalama, nishati na kilimo, pia katika upande wa elimu; ziara hiyo itaiwezesha Tanzania kupata fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Ethiopia, kubadilishana wanafunzi na kubadilishana uzoefu katika utengenezaji wa mitaala, na kuweka taratibu bora za kudhibiti uhamiaji holela.

Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie walioshirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na ni miongoni mwa viongozi waanzilishi 32 wa Umoja wa Afrika wakati huo OAU mwaka 1963.

Send this to a friend