APHFTHA yakubali kutoa huduma kwa wanachama wa NHIF

0
28

Uongozi wa Bodi ya Wamiliki wa Vituo vya Afya vya Binafsi (APHFTHA) na Jumuiya ya Wamiliki Hospitali Binafsi Zanzibar (ZAPHOA) umesema kufuatia Serikali kuonesha utayari wa kurudi katika meza ya mazungumzo kupitia mawasiliano yanayoendelea kati ya Serikali na APHFTHA wamefikia uamuzi wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Serikali na kurejesha huduma zilizositishwa kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Hatua hiyo ni kufuatia siku chache baada ya APHFTHA kutangaza kusitisha huduma kwa wagonjwa ambao ni wanachama wa NHIF kwa sababu zilizotolewa kuwa kitita kipya cha mfuko huo kilichotangazwa kutumika kuanzia Machi 1, 2024 hakiendani na uhalisia wa soko.

Tunawataarifu na kuwasihi watoa huduma kurejesha huduma hizo kuanzia leo Machi 02, 2024 hadi hapo tutakapowatangazia vinginevyo. Tunapenda kusisitiza kwamba lengo la APHFTHA na ZAPHOA ni kutoa huduma bora za afya katika mazingira ambayo yanazingatia hali ya soko na uhalisia wa gharama za uendeshaji za wamiliki wa vituo vya afya na hospitali. Kamwe, dhamira yetu si kuwaumiza wananchi na wahitaji ambao ni wanachama wa NHIF,” imesema taarifa ya APHFTHA.

Imeongeza, “uamuzi huu mgumu tunaochukua ni kielelezo cha nia yetu njema na dhamira yetu safi ya kutafuta suluhu ya kudumu itakayowaondolea wananchi adha ya kupata huduma za afya katika vituo vyetu na kutupunguzia wamiliki gharama za utoaji huduma na uendeshaji.”

Aidha, imesema kamati maalum ya APHFTHA itaundwa ili kushiriki majadiliano hayo ya kurekebisha bei zilizoleta mgogoro.

Send this to a friend