Mfahamu Dorothy Semu, kiongozi aliyemrithi Zitto Kabwe ACT-Wazalendo

0
74

Dorothy alizaliwa mwaka 1975 na wazazi waliokuwa watumishi wa umma na kukulia jijini Arusha na mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania.

Alipata shahada ya uzamili katika tiba ya mwili (Physiotherapy) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, Afrika Kusini, na baadaye akatumikia serikali kwa miaka 17.

Kazi zake zilihusisha kutibu wagonjwa na kusimamia programu za afya, hasa katika eneo la kudhibiti ulemavu wa ukoma.

Uzoefu wake wa kazi ulimwezesha kuboresha takwimu za kitaifa kuhusu huduma za afya kwa watu walioathiriwa na ukoma.

Dorothy aliamua kuchukua hatua zaidi katika kupigania usawa na kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuingia katika siasa ambapo alijiunga na chama cha ACT-Wazalendo na kufanya kazi kama Katibu wa Sera na Utafiti wa chama hicho.

Amefanya kazi kama Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo kati ya mwaka 2017 na 2020, kisha kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Bara ambapo amehudumu nafasi hiyo mpaka sasa.

Amekuwa Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo kuanzia mwaka 2020 mpaka mwaka 2022.

Machi 6, 2024 amechaguliwa kuwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo na akichukua nafasi ya Zitto Kabwe ambaye amemaliza muda wake.