Kufuatia mahojiano na pacha waliokuwa wakisoma Chuo Kikuu Ardhi wakieleza jinsi walivyoweza kufanyiana mtihani, uongozi wa chuo hicho umesema unafanya uchunguzi wa jambo hilo.
Katika mahojiano hayo ya Wasafi FM yaliyofanyika Machi 6 mwaka huu, pacha mmoja alikiri kumfanyia pacha mwenzake mtihani wa marudio (supplementary) wa Hydrolojia kwa kutumia kitambulisho cha mwenzake baada ya kufeli mtihani huo.
“Tulikuwa chuo sasa unajua chuo tunasoma kozi ambayo kuna masomo ambayo tunaendana kwahiyo sasa kuna somo moja ambalo linaitwa Hydrology tukawa tunaingia class moja lakini bahati mbaya mwenzangu akapata supp mimi nikawa nimetoboa, sasa nikamwambia hapo kwenye supp tulia nitafanya mimi [..] akanipa kitambulisho chake nikamaliza akatoboa supp na hawakuwahi kujua,” mmoja wa pacha alieleza.
Aidha, uongozi wa chuo hicho umesema baada ya kufanya utafiti na kubaini ukweli wa taarifa hizo, umma utajulishwa juu ya matokeo ya uchunguzi huo.