Indonesia inaichunguza ndege ya Batik Air baada ya marubani wote wawili kupatikana wakiwa wamelala kwa dakika 28 katikati ya safari.
Wanaume hao wawili ambao wote wamesimamishwa kazi kwa muda, walilala wakati wa safari Januari 25 kutoka Sulawesi kuelekea mji mkuu Jakarta ambapo mmoja wao aliripotiwa kuwa alichoka kutokana na kuwalea mapacha wake wachanga.
Ndege hiyo aina ya Airbus A320 iliacha njia kwa muda lakini ilitua salama, huku abiria wote 153 na wahudumu wote wakiwa salama.
Inaelezwa kuwa, rubani mwenye umri wa miaka 32 alimwambia rubani msaidizi mwenye umri wa miaka 28 kuchukua udhibiti wa ndege kwa takribani nusu saa baada ya kupaa ili aweze kupumzika kutokana na uchovu alionao, na rubani msaidizi alikubali lakini muda mfupi baadaye alisinzia pia.
Mamlaka ya anga ya Jakarta ilijaribu kuwasiliana na chumba cha marubani cha ndege ya Batik Air A320 lakini hawakutoa majibu kwa takribani dakika 28 hadi rubani kiongozi alipoamka na kugundua kuwa rubani mwenzake naye alikuwa amepitiwa na usingizi huku ndege ikiwa imeacha njia.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa kabla ya safari ulibaini kuwa marubani hao hawakuwa na shida yoyote ya kiafya kwani shinikizo lao la damu na mapigo ya moyo yalikuwa ya kawaida na vipimo vya pombe vilikuwa hasi.