Yanga yawasilisha malalamiko CAF kuhusu goli la Aziz Ki

0
57

Uongozi wa Yanga SC umeandika barua kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ukitaka uchunguzi ufanyike juu ya goli la Yanga lililokataliwa katika mchezo wa kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini.

Shuti hilo lililopigwa na mchezaji Aziz Ki dakika ya 57 ya mchezo kisha kukataliwa na refa Dehane Beida raia wa Mauritania, limezua mijadala mingi mtandaoni huku baadhi ya watu wakihoji kuwa kwanini VAR haikutumika kuhakiki kama ilikuwa ni goli ama si goli.

Barua ya Yanga kupitia Mkurugenzi wa Sheria, Simon Patrick imewalalamikia marefa kwa kushindwa kutumia teknolojia ya VAR kupata ufumbuzi licha ya kwamba waliweza kutumia teknolojia hiyo kuhakiki faulu ya mchezaji wa Yanga, Joyce Lomalisa.

Aidha, Yanga imeiomba CAF kutumia ushahidi wa rekodi za VAR ili kubaini ikiwa kuna viashiria vya upendeleo kwa Mamelodi vimefanyika, na ikijiridhisha kuwa kuna upendeleo ichukue hatua kwa kila aliyehusika, iweke hatua madhubuti za kudhibiti tukio kama hilo lisijirudie kwenye mechi zijazo, pia ichukue maamuzi mengine ambayo CAF itaona yanafaa chini sheria za mpira za CAF.

Send this to a friend